Government Emblem

The United Republic of Tanzania

Chuo cha Ustawi wa Jamii

Institute Logo

Menejimenti na Waratibu wa M&E Wajengewa Uwezo ISW

19 August 2026
Menejimenti na Waratibu wa M&E Wajengewa Uwezo ISW
Chuo cha Ustawi wa Jamii kimeendesha warsha ya kuwajengea uwezo viongozi wakuu wa taasisi, wakuu wa idara, kurugenzi, vitengo pamoja na waratibu wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E Champions) kuhusu Mwongozo wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E System Blueprint), kwa lengo la kuwawezesha kuanza kutekeleza mfumo huo pamoja na maandalizi ya awamu ya kwanza ya utoaji wa taarifa za robo mwaka. Warsha hiyo ilifanyika tarehe 21–22 Julai 2026 katika ukumbi wa Ofisi za NACTVET, jijini Dar es Salaam, na kuwezeshwa na Dkt. Kapongola Nganyanyuka. Akifungua warsha hiyo, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala, Dkt. Zena Mnasi Mabeyo, alisisitiza umuhimu wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini katika kuimarisha utendaji wa taasisi. Alisema, “Mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa chuo kinafikia malengo yaliyojiwekea katika Mpango Mkakati wa Sita na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.” Aidha, aliwataka washiriki kutumia maarifa watakayoyapata ili kuboresha ukusanyaji, uhakiki na matumizi ya takwimu kwa maendeleo ya chuo . Kupitia warsha hiyo, washiriki walitarajiwa kuelewa madhumuni na muundo wa Mwongozo wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Chuo cha Ustawi wa Jamii , kuhusianisha mfumo huo na Mpango Mkakati wa Sita pamoja na utendaji wa taasisi, kufafanua majukumu ya ukusanyaji, uhakiki, utoaji na matumizi ya taarifa, kutumia mbinu za msingi za kuhakikisha ubora wa takwimu kwa ajili ya taarifa za robo mwaka, na kubaini hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi cha utoaji wa taarifa za Julai hadi Septemba.
Institute Logo