Nyumba ya Sayansi na Utamaduni ya Ubalozi wa Urusi Yatembelea Chuo cha Ustawi wa Jamii, Yatangaza Fursa za Masomo Nchini Urusi
03 September 2026
Dar es Salaam, Julai 13, 2026 – Wanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii wamehimizwa kutumia fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa na Serikali ya Urusi ili kujiendeleza kitaaluma na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira la kimataifa. Wito huo ulitolewa na Meneja wa Programu wa Nyumba ya Sayansi na Utamaduni kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania, Bernad Sepetu, wakati wa semina maalumu iliyofanyika ISW tarehe 13 Julai, 2026. Semina hiyo ililenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu utamaduni wa Urusi pamoja na kuwafahamisha kuhusu fursa mbalimbali za masomo kupitia programu za ufadhili zinazotolewa na Serikali ya Urusi. Akizungumza katika semina hiyo, Sepetu alisema kuwa programu za ufadhili wa masomo zimekuwa zikiwapa wanafunzi wa Kitanzania nafasi ya kupata elimu ya kiwango cha kimataifa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Urusi, huku zikichangia kukuza ujuzi, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa. Alieleza kuwa mbali na kupata elimu bora, wanafunzi wanaonufaika na programu hizo hupata nafasi ya kujifunza lugha na utamaduni wa Urusi, kujenga mtandao wa kitaaluma na wa kimataifa, pamoja na kupata uzoefu unaowawezesha kuwa rasilimali muhimu katika maendeleo ya Tanzania. Katika semina hiyo, washiriki pia walipata maelezo kuhusu historia, mila na desturi za Warusi, mfumo wa elimu wa nchini humo, pamoja na hatua na vigezo vinavyotumika kuomba nafasi za ufadhili wa masomo kupitia Nyumba ya Sayansi na Utamaduni kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania. Wanafunzi walitumia nafasi hiyo kuuliza maswali mbalimbali kuhusu taratibu za maombi, aina za kozi zinazotolewa, maisha ya wanafunzi nchini Urusi na fursa zinazopatikana baada ya kuhitimu masomo. Kwa upande wao, wanafunzi walieleza kufurahishwa na semina hiyo, wakisema imewapa uelewa mpana kuhusu Urusi na kuwafungua macho kuona fursa za masomo ya kimataifa ambazo zinaweza kuwasaidia kufikia malengo yao ya kitaaluma na kitaifa. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Tanzania na Urusi, huku Chuo cha Ustawi wa Jamii kikiendelea kuwahamasisha wanafunzi wake kutumia fursa mbalimbali za masomo na mafunzo zinazopatikana ndani na nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa.