ISW na Coca-Cola Kwanza Wasaini Makubaliano ya Kuimarisha Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana na Wanawake
03 September 2026
Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Coca-Cola Kwanza Limited (CCK), Julai 20, 2026, zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano wa miaka mitano inayolenga kuwawezesha kiuchumi vijana na wanawake wanaojishughulisha na biashara za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini. Makubaliano hayo yalisainiwa na Dkt. Joyce Nyoni, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, kwa niaba ya ISW, na Maria Kimwaga, Mkuu wa Mahusiano ya Umma na Uendelezaji, kwa niaba ya Coca-Cola Tanzania. Ushirikiano huo utatekelezwa kupitia programu za "Mwanamke Shujaa" na "Chipsika na Coke", zikiwa na lengo la kupunguza umaskini, kuongeza fursa za ujasiriamali, na kuboresha maisha ya wanufaika. Kupitia makubaliano hayo, mafunzo ya ujasiriamali yatatolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tanga, Mtwara, Lindi, Mbeya na Songea. Mafunzo hayo yatajumuisha usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, huduma kwa wateja, ukuaji wa mitaji, pamoja na afya ya akili na huduma za msaada wa kisaikolojia. Aidha, wanufaika watapatiwa vifaa muhimu vya biashara, ikiwemo meza, viti vya wateja, mitungi na majiko ya gesi, aproni, fulana, pamoja na kreti za vinywaji, ili kuboresha na kukuza shughuli zao za kiuchumi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Coca-Cola Kwanza itagharamia uratibu wa shughuli, utoaji wa vifaa vya biashara, pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa programu. ISW, kwa upande wake, itatoa wataalamu wa mafunzo ya ujasiriamali, kufanya utambuzi wa wanufaika, na kuandaa taarifa za utekelezaji. Pande hizo mbili pia zitafanya tathmini ya maendeleo ya programu kila baada ya miezi sita ili kupima matokeo na kuhakikisha malengo ya kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalumu yanatekelezwa kwa ufanisi katika kujenga uchumi shirikishi na endelevu nchini.