FURSA ZA UFADHILI ELIMU YA JUU NCHINI URUSI
12 November 2026
Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) tarehe 10 Novemba, 2026 kilipata heshima ya kuwa miongoni mwa vyuo vya elimu ya juu nchini kutembelewa Wakuu wa Vyuo (Rectors) na wawakilishi kutoka vyuo vikuu kumi vya Urusi wakati wa ziara ya kutangaza fursa ya Elimu ya juu Urusi nchini Tanzania inayoendelea kuanzia tarehe 9–13 Novemba 2026.
Vyuo hivyo ni Plekhanov Russian University of Economics, Southern Federal University, Siberian State University of Engineering and Biotechnology, Samara Polytech, Saint Petersburg University, RUDN University, Samara State University of Social Sciences and Education, Moscow State University of Technology “STANKIN”, Tula State University na Tomsk State University.
Ziara hiyo imefungua fursa muhimu kwa wanafunzi wa Kitanzania na hasa wa #ISW kupata ufadhili wa masomo nchini Urusi, kujiendeleza na elimu ya juu, kushiriki programu za kubadilishana wanafunzi na watumishi, kufanya tafiti za pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi. Aidha, ziara hii imeendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano baina ya Tanzania na Urusi kupitia sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wageni hao, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni aliwashukuru kwa ziara hiyo na kusisitiza utayari wa ISW kujenga ushirikiano endelevu. Aliahidi kuendeleza mawasiliano ya karibu kupitia Ofisi ya Umataifishaji (Internationalization Office) ili kutambua na kuratibu fursa zaidi za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.