Dkt. Joyce: Familia imara msingi wa taifa lenye ustawi
09 March 2026
Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni Mkuu amesema familia ni taasisi ya kwanza ya kijamii ambayo binadamu huikuta kabla ya shule, kanisa au msikiti na ajira. Aidha,amesema ndani ya familia ndipo mtoto hujifunza lugha, maadili, heshima pamoja na kujifunza namna ya kuishi na wengine. "Tunaposema familia yangu, Taifa langu” tunamaanisha kuwa ubora wa Taifa ni kioo cha ubora wa familia zake,"alisisitiza. Dkt.Joyce ameyasema hayo leo Machi 6,2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu familia yangu Taifa langu katika Kongamano la Wanawake 2026 lililoandaliwa na Shirika la Utangazaji (TBC) kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani katika Ukumbi wa Mkataba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum, Mh. Dkt.Dorothy Gwajima. "Ikiwa familia zetu zina amani, Taifa litakuwa na amani Ikiwa familia zetu zina misingi ya haki, Taifa litakuwa na misingi ya haki,ikiwa familia zetu zina usawa, Taifa litakuwa jumuishi,"amesisitiza. Aidha,amesema kuwa amani ya Taifa huanzia kwenye amani ya familia na kwamba familia yenye migogoro, dhuluma na ukatili huathiri afya ya akili ya watoto. "Watoto wanaokulia katika mazingira ya vurugu wana uwezekano mkubwa wa kuendeleza vurugu, kukosa utulivu wa kisaikolojia, kushindwa kufikia uwezo wao wa juu,"amesema ambaye kitaalum ni Daktari wa Sosholojia.