Chuo cha Ustawi wa Jamii

Maendeleo ya Kasi Kampasi ya Kisangara

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amekipongeza Chuo cha Ustawi wa Jamii kwa Maendeleo ya kasi yanayoendelea katika Kampasi ya Kisangara. Wakili Amon Mpanju ametoa pongezi hizo wakati wa Mahafali ya 6 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara, Mwanga Kilimanjaro Januari 26, 2024. ambapo jumla ya wahitimu 237 wametunukiwa tuzo mbalimbali. "Naipongeza pia Menejimenti ya Chuo kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Hostel mbili zenye ukubwa wa kubeba wanafunzi 208, ujenzi wa mgahawa kwa matumizi ya wanafunzi na jamii nzima inayozunguka chuo. Nawapongeza pia kwa juhudi ambazo mmezichukua za kuhakikisha maji yanapatikana katika eneo letu la Chuo. Hakika hii itaifanya Kisangara iendelee kuwa ya kijani zaidi." Amesema Mpanju. Mpanju pia amefurahishwa na kuanzishwa kwa kozi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa ngazi ya cheti na diploma ambayo inatambuliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kuanzishwa kwa programu ya Shahada ya Ustawi wa jamii (Bachelor Degree in Social Work) inayotambuliwa na Tume ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) katika mwaka wa masomo 2023/2024 Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdalah Mwaipaya akizungumza katika mahafali hayo amesema uwepo wa chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara ni muhimu kwa wilaya ya mwanga kwa kuvutia zaidi uwekezaji. Amewaasa wanafunzi kurudi Mwanga Kuendelei kusoma Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara. Naye Naibu Kamisha wa Ustawi wa Jamii Tullo Masanja amewakumbusha wahitimu kuwa ndiyo madaktari wa jamii kutokana na ongezeko la tatizo la afya ya akili, hivyo wanatakiwa kutumia utaalamu waliopata kuhakikisha wanalinda na kuokoa jamii, hasa mmomonyoko wa maadili. Dkt. Lulu Mahai (Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo) Ameeleza Jinsi ambavyo kampasi inakabiliwa na changamoto ya jengo la utawala na ufinyu wa jengo la maktaba ukizingatia ongezeko la wanafunzi baada ya kuongeza Programu mbili za Kitaaluma katika kampasi hiyo.

Mh. KASSIM MAJALIWA AKIPONGEZA CHUO CHA USTAWI WA JAMII KWA KAZI NZURI

Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekipongeza Chuo cha Ustawi wa Jamii kwa kuzalisha wataalamu ambao wanashughulikia changamoto mbali mbali za makundi maalum nchini. Waziri Mkuu ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii na wiki ya Ustawi wa Jamii yaliyofanyika Dar es Salaam tarehe 18/12/2023 katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere. Mh. Waziri Mkuu amewataka Wazazi, Wazlezi na Jamii kwa ujumla kuhakikisha wanadumisha ustawi wa watoto kwa kuwa ndio mustakabali wa wa taifa. Wakati huo huo Waziri Mkuu ameipongeza wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Kushirikiana na TCRA na Wizara wa Habari na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana kuanzisha vipindi vya Redio ambavyo vimelenga kuelimisha Jamii juu ya malezi ya watoto na vijana. Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika Chuo kupitia kituo cha ubunifu, kimebuni program tumizi ya kusaidia jamii ambayo ni mfumo uliotengenezwa na wanafunzi wa chuo cha ustawi wa Jamii kwa wanajamii kutoa ripoti za Masuala ya Ukatili na Kuyafikisha kwa maafisa ustawi wa Jamii wa maeneo husika ili kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Dr. Joyce Nyoni amesema Chuo kupitia kampasi ya kisangara kimejielekeza kuwa kituo cha umahiri cha kutoa mafunzo ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto ili kusaidia kuiandaa jamii mapema katika kuboresha makuzi na Malezi ya awali ya watoto na Vijana. Pia, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amempongeza Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni kwa usimizi imara wa Chuo cha Ustawi wa Jamii. Chuo cha Ustawi wa Jamii kimefikia kilele cha Maadhimisho ya miaka yake 50 Tangu kilipoanzishwa mwaka 1973.

Mhe.Dkt.Dorothy Gwajima atunuku tuzo mbali mbali katika mahafali ya 47 ISW

Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum tarehe 8 Desemba, 2023 ametunuku tuzo mbali mbali kwa wahitimu katika Mahafali ya 47 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam. Katika mahafali haya wamehitimu wanafunzi 2,936 kati ya hao 1705 sawa na silimia 58 ni wanawake na 1327 sawa na asilimia 42 ni wanaume.

KONGAMANO LA 10 LA KITAALUMA LAJADILI ujenzi wa ujuzi na ushirikishwaji wa watu wenye wenye mahitaji maalum katika shughuli za maendeleo

Wadau, wanataaluma na wanafunzi wameshiriki katika kongamano la 10 la kitaaluma (Convocation) juu ya ujenzi wa ujuzi na ushirikishwaji wa watu wenye wenye mahitaji maalum katika shughuli za maendeleo. Akizungumza leo Desemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano hilo , Naibu Mkuu wa Chuo Prof.Sotco Komba Taaluma amesema chuo kimejikita zaidi katika maboresho ya watu wenye ulemavu ili kukuza ujuzi katika nyanja ya maendeleo ya kiuchumi ili waweze kushirikia michakato mbalimbali ya maendeleo katika taifa letu. Dkt. Nassib Mwaifunga, mtaalam wa masuala ya Uchumi na Fedha na Sheria kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali kutoka ofisi ya Waziri Mkuu hasa walemavu ili waweze kujikomboa kiuchumi na kukuza maeneleo katika maisha yao ya kila siku. Aidha aliwataka vijana ambao ni wanafunzi kwenda na wakati katika mafunzo na masomo wanayochukua ili waweze kwenda na kasi ya soko la ajira duniani. Amebainisha fursa kubwa hasa ajira ambazo zinapewa kipaumbele kwa kuzingatia ujuzi iko katika kiwango kikubwa katika kozi za mafuta na gesi, usafirishaji, afya na vifaa tiba na madini. Mbali na hilo amewataka waajiri nchini kuachana na dhana ya kudharau watu wenye mahitaji maalum hasa katika kuwapa ajira kwani watu hao wana uwezo mkubwa wanapopewa nafasi. #chuochaustawiwajamii kimepongezwa kwa kuanzisha kitengo maalum utoaji wa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine nchini Umekuwa ni utamaduni wa Chuo cha Ustawi wa Jamii kufanya kongamano hili la kitaaluma kila mwaka kabla ya mahafali yake, ambapo kwa mwaka 2023 mahafali hayo yatafanyika tarehe 08/12/2023 katika ukumbi wa JKT mwenge.

ISW Yashinda Tuzo Uandaaji Taarifa za Hesabu za mwaka 2022

Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce nyoni akiwa pamoja na baadhi ya wahasibu wa #ISW akipokea tuzo ya mshindi wa tatu ya uandaaji wa taarifa za hesabu chini ya viwango vya IPSASs 2022, katika kundi la vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mara nyingine. Tuzo hiyo imetolewa jioni ya tarehe 1, Disemba 2023 na NBAA katika hafla maalum ya kutoa tuzo hizo.

BONANZA LA MICHEZO KUELEKEA KILELE CHA MIAKA 50 LAZINDULIWA

Dkt. Happy Mwakajila kwa Niaba ya Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni amefungua Bonanza la Michezo ikiwa ni sehemu ya shughuli mbali mbali kuelekea Kilele cha Miaka 50 ya Chuo ambapo timu ya Mpira wa Miguu ya Wanaume #ISW imepimana nguvu na timu ya watumishi wa Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam ambapo timu zote mbili zimetoka sare ya bila kufungana katika mechi hiyo. Michezo hiyo itakutanisha Taasisi na vyuo mbali mbali ikihusisha wanafunzi na watumishi katika michezo mbali mbali.

NAIBU KATIBU MKUU WAKILI AMON MPANJU AFANYA KIKAO KIFUPI ISW

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amefika katika Chuo cha Ustawi wa Jamii leo tarehe 10/11/2023 na kukutana na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya chuo ili kupata taarifa ya hali ya utoaji huduma, maendeleo ya miradi ya chuo na vile vile kutoa maelekezo na ushauri katika kuboresha utoaji huduma na utekelezaji wa miradi ya chuo.

CHUO CHA USTAWI WA JAMII CHAFANYA MAWASILISHO YA TAFITI ZA KITAALUMA.

Chuo cha Ustawi wa Jamii leo tarehe 10/11/2023 kimefanya mawasilisho ya tafiti mbili za kitaaluma ambazo imezifanya katika mada mbili tofauti ikilenga kutafuta kina cha suluhu ya matatizo ya hali mbali mbali yanayotokea katika jamii ya kitanzania. Akiwasilisha taarifa za tafiti hizo mmoja wa mtafiti kiongozi wa tafiti hizo Mhadhiri Mwandamizi Dkt. Zena Mabeyo amesema wamefanya tafiti mbili ambazo ni: - ‘’kuchunguza kanuni, maadili na mbinu zinazowalinda wanawake dhidi ya unyanyasaji Tanzania: uchunguzi kesi ya mikoa ya Mbeya, Mara na Tanga’’ na kuathirika kwa wafanyakazi wasio rasmi katika muktadha wa Uviko 19: kesi ya sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro na Arusha. Kwa taarifa Zaidi tembelea ; https://www.isw.ac.tz/assets/doc/Dissemination_brief_PROWOMEN.pdf, https://www.isw.ac.tz/assets/doc/REPOA_FINAL_EDITED_POLICY_BRIEF_07_11_2023_(1).pdf

KARIBUNI - ISW

Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni amefungua Mafunzo ya awali kwa watumishi wapya ISW. Akiongea katika ufunguzi wa mafunzo hayo katika kampasi ya Dar es Salaam, Dkt. Joyce amewapongeza watumishi hao wapya na kuwaasa kuwa waadilifu, wachapakazi, kufanya kazi kwa weledi, na kutoa huduma bora kwa wateja wa Chuo cha Ustawi wa Jamii.

Mkuu wa Chuo ISW Aongea na Wanafunzi wapya

Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni amezungumza na Wanafunzi wapya wa Chuo cha Ustawi wa Jamii ambao wanatarajiwa kuanza mwaka wa masomo 2023/2024 katika wiki ya mafunzo ya awali na usajili ambayo inaendelea Chuoni hapa. Amewapongeza kwa kuweza kuchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya Juu na hasa Chuo Cha Ustawi wa Jamii. Dkt. Joyce alisema tunatamani kuwa na ninyi mpaka mwisho wa Programu zenu za masomo yaan kutoka Cheti, Diploma mpaka Degree. "Tufike mwisho wa safari kwa ushindi bila majeraha, majeraha ni kurudia somo au kufeli somo na kulibeba mwaka unaofuata. Mimi nilimaliza Masomo yangu bila Kufeli Somo na ninyi mnaweza" alisema Dkt. Joyce Tuweke malengo ya kumaliza bila majeraha,tumalize shule kwa wakati ili tusiwape mzigo wazazi na walezi wetu ambao wana tuwezesha kulipa ada na mahitaji tukiwa masomoni. Kama Chuo tuna ahidi kuwapa huduma stahiki, za kitaaluma na Kiutawala, nawasihi sana tumieni vizuri ofisi zetu kupata ushauri pale mnapopata changamoto zozote, tuna Kituo cha Elimu,Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia, Ofisi ya Mshauri wa wanafunzi, Dawati la Jinsia, pamoja na Ofisi za Wakuu wa Idara zenu, muwe huru kwenda kupata huduma. Mwisho nawaomba muwe mabalozi wazuri wa Chuo chetu, Mvae vizuri, Muwe nadhifu, na Muongee vizuri na Jamii yenu kama wasomi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii

KOICA, ISW WAKABIDHIANA NA KUZINDUA VIMBWETA

Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA Tanzania Mr. Manshik Shin na Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni tarehe 04, Oktoba 2023, wamekabidhiana na kuzindua matumizi ya vimbweta vipya vilivyojengwa katika eneo cha Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Dar es Salaam. Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika baada ya ujenzi wa vimbweta hivyo kukamilika ambapo KOICA kupitia mradi wao wa kujitolea ulifanikisha kujengwa kwa vimbweta hivyo vya kisasa ambavyo vitapunguza uhaba wa sehemu za kujisomea wanafunzi wakisubiri vipindi au wakati wa mitihani. KOICA kwa muda sasa imekuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa Chuo cha Ustawi wa Jamii ambapo mpaka sasa wameshafanya miradi kadhaa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya utoaji huduma katika chuo cha ustawi wa jamii.

Site Visitors
Today
936
Yesterday
815
This Week
8,863
This Month
34,471
All days
178,346
Online
10
Video